Tuesday, October 2, 2012

ANGALIA JINSI AJALI ILIYOTOKEA MBEYA LEO ILIVYOUA WATU 10 NA KUJERUHI WENGINE KIBAO... MBUNGE MARY MWANJELWA ANUSURIKA KIMIUJIZA HUKU GARI LAKE LIKITEKETEA VIBAYA KWA MOTO... MIILI MINGINE HAITAMBULIKI KWANI IMEUNGUA VIBAYA NA KUBAKI VIPANDE... KAMANDA WA POLISI MBEYA ASEMA DEREVA WA LORI LA MAFUTA LILILOSABABISHA AJALI HIYO WANAENDELEA KUMSAKA KWANI KAKIMBILIA KUSIKOJULIKANA... !

Wananchi wakiangalia mabaki ya gari alilokuwa Mhe. Mwanjelwa
Lori lililosababisha ajali Mbeya llilivyoteketea leo

Harakati za kuzima moto zikiendelea.

Mhe. Mary Mwanjelwa
Watu 1o wamefariki dunia na wengine 25 kujeruhiwa akiwamo Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa Mbeya (CCM), Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa baada ya ajali mbaya iliyotokea leo katika eneo la Mbalizi mkoani Mbeya na kuhusisha magari manne ambayo yote yaliteketea kwa moto.

Diwani Athumani ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya amesema kuwa miili ya watu nane iko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na mingine iko katika Hospitali ya Ifisi iliyopo katika Wilaya ya Mbeya Vijijini huku majeruhi wengine wakiwa pia katika hospitali hizo. Mhe. Mwanjelwa amelazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, ajali hiyo imetokea leo saa 7:00 mchana katika eneo la Mlima Iwambi kuelekea Mbalizi ambapo lori la mafuta lenye namba  IT 9518 lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Tunduma lilipoteza uelekeo na kugonga gari dogo la abiria aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T587 AHT na garia aina ya Toyota Hilux, namba za usajili  T671 ABM ambalo ni la Mbunge Mwanjelwa.

Imeelezwa kuwa lori hilo la mafuta lilianza kugonga lori moja ambalo halikupinduka, kisha likagonga magari hayo mengine mawili likiwamo la mbunge ambayo yote yalitumbukia kwenye korongo na baada ya hapo, lori hilo lenye mafuta liliripuka moto na kuunguza pia magari mengine na kuyateketeza huku yakisababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 25. Wengine waliokufa walikuwa ni wapita njia na mtu mmoja aliyekuwa na pikipiki.

Imeelezwa kuwa mbunge Mwanjelwa na watu wengine waliokuwamo kwenye magari hayo walinusurika kimiujiza tu kwani moto mkubwa uliotokana na kulipuka moto kwa lori lililosababisha ajali ulikuwa mkubwa na wa kutisha.

"Hivi sasa bado tunaendelea kumsaka dereva wa lori lililosababisha ajali ili tumkamate na kumhoji," amesema Kamanda Diwani Athumani.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alifika katika eneo la tukio na ametoa pole kwa wafiwa kisha akaelekea Hospitali ya Ifisi Mbalizi kwa ajili ya kuwajulia hali majeruhi akiwemo Mhe. Mwanjelwa.

Imefahamika kuwa dereva wa Mbunge Mwanjelwa aitwaye Rajabu ambaye alipelekwa katika Hospitali ya Ifisi ameumia vibaya kichwani na miguuni huku katibu wa Mbunge akipoteza maisha baada ya kuteketea kwa moto.

No comments:

Post a Comment