Nenda kwa yaliyomo

Silika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa dioksidi ya silikoni angalia hapa silika (kemia)

Silika ya nafsi ni jumla ya maelekeo ya ndani ya mtu yanayotokana na urithi, mazingira na utashi na ambayo yanaonyesha namna yake maalumu ya kuwaza na kujitokeza.

Upambanuzi wa silika za nafsi

[hariri | hariri chanzo]

Silika ni nyingi, kiasi kwamba toka zamani wataalamu wamejaribu kuzipambanua wasikubaliane. Baadhi yao wanasisitizia mwili kama msingi wa silika (k.mf. ya watu warefu wembamba, ya watu wafupi wanene, ya watu wenye umbo la wastani). Mtazamo huo una ukweli fulani, yaani umoja wa binadamu kama changamano la mwili na roho, lakini nafsi inaundwa zaidi na matukio ya maisha, hasa ya utotoni: ndiyo yanayomuathiri mtu zaidi, pamoja na kwamba anapaswa kurekebisha daima silika yake. Kwa ajili hiyo ni muhimu ajifahamu ili akuze sifa njema na kupunguza kasoro zake. Katika kazi hiyo ategemee sana msaada wa Mungu: neema ina nguvu kuliko maelekeo yoyote ya umbile na inatenda maajabu, tunavyoona katika maisha ya waliofikia utakatifu kuanzia silika tofauti kabisa. Neema haikomeshi umbile, bali inalikamilisha.

Hapa tutadokeza aina mbalimbali za upambanuzi, kuanzia ya zamani zaidi, kwa kufuata tu maelezo makuu yanayokubaliwa na wengi. Kila aina inafaa zaidi kwa baadhi ya watu, yaani wale wanaolingana wazi na taswira yake mojawapo; kumbe ni vigumu zaidi kutambua na kupanga wale wenye silika za wastani. Hapo ni afadhali kukimbilia aina nyingine ya upambanuzi. Kwa vyovyote si rahisi kupata mtu anayelingana na taswira fulani kwa asilimia mia: kwa kiasi fulani kila mmoja anaelekea taswira nyingine pia.

Aina za silika kadiri ya Wagiriki

[hariri | hariri chanzo]

Labda asili ya upambanuzi huu ni mganga Hipokrate (aliyekufa mwaka 377 K. K.). Zamani walidhani silika nne za msingi walizoziainisha zinategemea kile kinachotawala mwili wa mtu, yaani nyongo, neva, damu au limfu. Dhana hiyo haikubaliki tena, lakini wengiwengi wanafuata bado upambanuzi huo kadiri ya jambo linalojitokeza zaidi katika silika ya mtu, yaani hasira, huzuni, uchangamfu au upole.

Msingi wake ni jinsi yanavyochanganyikana kwa namna tofauti mambo mawili: wepesi wa kuhemka na elekeo la kutenda.

Aliye na yote mawili kuliko kawaida ni mtu wa hasira. Aliye na lile la kwanza kuliko kawaida lakini la pili kidogo kuliko kawaida ni mtu wa huzuni. Aliye na lile la kwanza kidogo kuliko kawaida lakini la pile kuliko kawaida ni mtu wa uchangamfu. Hatimaye aliye na yote mawili kidogo kuliko kawaida ni mtu wa upole.

Kwa kujibu maswali kadhaa tunaweza kujua tunayo kwa asilimia ngapi, na hivyo tunalingana na taswira mojawapo kwa kiasi gani.

Kila silika inapakana na nyingine mbili ambazo zinafanana nayo upande wa wepesi wa kuhemka au upande wa elekeo la kutenda, kumbe ni kinyume cha ya nne ambayo hailingani nayo wala upande wa wepesi wa kuhemka wala upande wa elekeo la kutenda.

Aina za silika kadiri ya sufii

[hariri | hariri chanzo]

Upambanuzi huu pia ni wa zamani, ila mwishoni mwa karne XX imechunguzwa na kutengenezwa upya na wanasaikolojia waliouita enneagram, yaani mchoro wa silika tisa, ambazo zinaitwa kwa tarakimu fulani na kupangwa katika duara. Hizo zinahusiana kwa namna mbalimbali, lakini hasa ni kwamba tatu (5, 6, 7) zinafuata zaidi mawazo ya kichwa, tatu (2, 3, 4) hisi za moyo, na tatu (8, 9, 1) misukumo ya matumbo. Kila mtu anaweza kutumia vitovu vyote vitatu, lakini polepole amependelea kimojawapo hata kikatawala vingine. Hivyo kwa kutegemea urithi na mazingira amepoteza uwiano.

Hakuna namba nzuri au mbaya zaidi: kila moja ina utajiri na udhaifu wake. Tusichague namba fulani kwa sababu tunaipenda, bali tujaribu kujua na kupokea ukweli juu yetu.

Aina za silika kadiri ya Carl Gustav Jung

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya michango mikubwa aliyoitoa mtaalumu huyo wa Uswisi (1875-1961), mmojawapo ni kuainisha makundi mawili ya watu kadiri wanavyoelekeza nguvu za nafsi yao ndani mwao (wandani) au nje yao (wasondani).

Watu wa makundi hayo yote mawili katika utendaji wana kawaida ya kutumia zaidi ama mawazo (mantiki), ama miguso (hisi za moyoni), ama hisi za nje (milango ya fahamu) ama machale (kuona mbali). Hivyo tunapata aina nane za silika (2x4).

Utambuzi wa silika kwa njia ya mwandiko

[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wengine hawakubali aina hizo za upambanuzi wa silika, wakidai zinalinganisha watu bila ya kujali tofauti nyingi zilizopo kati ya kila mmoja na wengine wote. Hao wanasisitiza kuwa watu ni mbalimbali kama alama za vidole vyao, yaani silika ya kila mtu ni ya pekee. Kazi yetu ni kuitambua kinaganaga, badala ya kuilazimisha ndani ya fremu fulani. Mwenendo mzima wa mtu, hasa asipotenda kwa [[makusudi, unamtambulisha (k.mf. mwendo wake wa kasi au wa taratibu, wa kelele au wa kimyakimya, n.k.).

Tangu zamani sana, watu kadhaa wa China, India, Ugiriki na Italia walivutiwa na jinsi mwandiko wa kila mmoja ulivyo tofauti na ule wa wengine, wakaona unadokeza nafsi yake. Kuanzia karne XVII vilianza kutungwa vitabu kuhusu suala hilo, mpaka ikakubalika sayansi ya mwandiko (grafolojia) inayochunguza uhusiano kati ya mwandiko wa mtu na undani na nafsi yake (akili, maelekeo, vipawa, umbo, maradhi n.k.). Msingi wake ni kwamba hatuandiki kwa mkono tu, kwa kuwa huo unaongozwa na ubongo. Mtu anapoacha kuiga herufi alizofundishwa kwa kuwa amezoea kuandika, anakuja kutokeza nafsi yake mwenyewe katika upekee wake. Tunaweza kusema mtu anapoandika bila ya kuzingatia usanifu wa herufi anajichora jinsi alivyo.