Namna siasa zinavyochangia matatizo ya umeme Tanzania
- Author, Na Damas Lucas
- Nafasi, Mchambuzi wa habari za uchumi na siasa
Waziri wa Nishati wa Tanzania, January Makamba amesema hivi karibuni kuwa matatizo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini Tanzania yataendelea hadi hapo ukarabati wa miundombinu ya kusafirisha nishati hiyo utakapomalizika.
Kauli hiyo inaonyesha jinsi tatizo la umeme nchini Tanzania lilivyo kubwa na jinsi ambavyo ahadi zilizotolewa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) kuhusu tatizo la umeme kuwa historia zilivyokuwa na siasa au tatizo la umeme kutumika kukidhi malengo ya kisiasa.
Mgombea urais wa CCM, John Magufuli (sasa marehemu) alisema kwenye kampeni za uchaguzi mwaka 2015 kwamba kama angechaguliwa, kukatika kwa umeme kungesahaulika.
Lakini sasa waziri Makamba anasema ni wajibu wake kuwaambia wananchi ukweli kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme nchini Tanzania: "Hatutawadanganya Watanzania kuhusu yaliyopo, tukifanya hivyo, tutakuja kuumbuka huko mbele na hatutazitendea haki nafasi tulizopewa," Gazeti la Mwananchi limemnukuu Makamba akisema alipokuwa akiongea na waandishi wa habari, Alhamisi, 24 Machi kuhusu mafanikio ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka mmoja.
Pamoja na ukweli mchungu wa kauli ya Makamba, ni wazi kuwa si Watanzania wengi watakaoshangazwa nayo. Kukatika kwa umeme mara kwa mara ni tatizo ambalo limezoeleka nchini Tanzania kiasi kwamba si tukio kubwa la kuripotiwa na vyombo vya habari hasa vya kimataifa pale linapotokea.
Linganisha na hali ilivyo katika nchi jirani ya Kenya. Tarehe 11 Januari mwaka huu wa 2022 umeme ulikatika kwa saa kadhaa katika nchi nzima ya Kenya baada ya njia ya umeme yenye msongo mkubwa kati ya Nairobi na bwawa la kufua umeme la Kiambere kupata hitilafu.
Tukio hilo liliripotiwa si tu na vyombo vya habari vya ndani lakini pia na vyombo vya habari vya kimataifa. Ilikuwa ni mara ya tatu ndani ya miaka minne kwa tatizo kama hilo kutokea. Vyombo vya habari vilitangaza kuwa tukio kama hilo lilitokea kwa mara ya mwisho mwezi Mei mwaka 2020. Baada ya tukio hilo viongozi waandamizi tisa wa kampuni ya Kenya Power inayosambaza umeme nchini Kenya walifikishwa mahakamani kwa kushindwa kuzuia uharibifu wa njia ya umeme.
Kwa hapa nchini Tanzania kama kuna kazi ngumu anayoweza kupewa mtu kuifanya ni kuhesabu mara ngapi umeme unakatika nchini Tanzania kwa mwezi au hata kwa juma moja. Hakika ni kazi ngumu.
Na waziri Makamba anasema chanzo cha kukatika kwa umeme mara kwa mara ni miundombinu mibovu ya kusambaza umeme ambayo haikufanyiwa matengenezo kwa miaka mingi.
Februari 15, 2022 wakati akijibu hoja za wabunge katika mkutano wa 16 wa Bunge mjini Dodoma, waziri Makamba alielezea kwa kina kuhusu tatizo na hatua ambazo serikali inazichukua kulitatua.
Lakini baadhi ya wabunge walikataa maelezo ya waziri wakidai kuwa kuna jambo lililofichika nyuma ya pazia kuhusu tatizo la umeme. Walidai kuwa kuwa kipindi ambacho Makamba anasema miundombinu ya umeme ilikuwa haifanyiwi ukarabati umeme ulikuwa haukatiki hovyo.
Siasa katika sekta ya umeme Tanzania
Kukatika kwa umeme ni matokeo ya siasa ambazo zimesababisha maamuzi makubwa ya kitaalam yafanyike kisiasa.
Hata mjadala mkali kuhusu umeme uliotikisa Bunge la Januari, 2022 nao ulikuwa wa kisiasa zaidi. Ulitawaliwa na mashambulizi ya kisiasa ya mojamoja na vijembe dhidi ya waziri Makamba kana kwamba waziri huyo ndiye chanzo cha kukatika kwa umeme.
Baadhi ya wabunge walitaka kuonesha kuwa tatizo la kukatika kwa umeme lilikuwa limekwisha ila limerudi tu baada ya waziri Makamba kuanza kuongoza wizara ya Nishati, suala ambalo si kweli.
Ilivyo bahati, takwimu alizotoa mbunge wa Viti Maalamu, Jesca Kishoa wakati akichangia bungeni zilionesha kuwa tatizo la kukatika kwa umeme halijawahi kwisha. Mbunge Kishoa alisoma bungeni taarifa ya mwaka 2018 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) iliyoonesha kuwa mwaka 2017 umeme ulikatika mara 2,844 nchini Tanzania. Hii inamaanisha mwaka 2017 umeme ulikatika takribani mara saba kwa siku. Hiki ndiyo kipindi ambacho baadhi ya wabunge wanadai umeme ulikuwa haukatiki.
Siasa katika sekta ya umeme nchini Tanzania hazikuanza mwaka huu. Zilianza tangu wawekezaji binafi waliporuhusiwa kuzalisha umeme mwanzoni mwa miaka ya 1990. Baadhi ya kampuni za wazalishaji binafsi wa umeme (Independent Power Producers) zilizoingia Tanzania zilikuwa ni IPTL, Richmond na Dowans. Wengi wa wazalishaji hawa huru walihusishwa na siasa za chama tawala, CCM. Lakini kuja kwao kuligubikwa na tuhuma za rushwa zilizosababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa mwanzoni mwa 2008. Hata hivyo Lowassa akizungumza Bungeni kabla ya kujiuzulu, alilalamika kuwa alionewa kwa kutuhumiwa na kuhukumiwa bila kusikilizwa, hivyo alijiuzulu ma maslahi ya chama chake na serikali.
Ni wazi kuwa siasa zilichochewa na sekta hiyo kuwa chanzo kikubwa za cha fedha za dhuluma kwa wanasiasa waroho na wasiokuwa waaminifu. Hata vita vya kisiasa vilivyopiganwa bungeni Januari, 2022 zinaonyesha zinaweza kuhusishwa na hisia za ulaji wa fedha za umma katika sekta ya umeme.
Matokeo ya maamuzi kufanyika kisiasa ni kuwa mikataba yenye kasoro iliyoingiwa kati ya serikali na wazalishaji huru wa umeme ilifanya shirika la umeme nchini Tanzania, Tanesco, linunue umeme kwa bei za juu kutoka kwa wazalishaji hao. Jambo hili lilisababisha gharama kubwa za uendeshaji zilizozuia ukarabati wa miundombinu wa mara kwa mara. Majaribio ya serikali kuvunja mikataba yalisababisha kesi za muda mrefu mahakamani.
Fursa adimu
Tanzania ilishindwa kutumia ipasavyo fursa adimu ya kurekebisha sekta ya umeme nchini (eletricity sector reforms) mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Nchi ya jirani ya Kenya iliyoitumia fursa hii vizuri iliondokana na matatizo ya kukatika umeme kila siku. Kenya ilichukua hatua za haraka kutenganisha shughuli za uzalishaji wa umeme na zile za usafirishaji na ugavi.
Mwaka 1998 serikali ya Kenya iliunda shirika la uzalishaji umeme, KenGen na kuuza asilimia 30 ya hisa zake za KenGen kwa wananchi kupitia Soko la Hisa. Shirika hili ambalo linazalisha asilimia 65 ya umeme nchini Kenya linajiendesha kwa ufanisi mkubwa kwa sababu linawajibika kwa wanahisa walio wengi zaidi.
Kuundwa kwa KenGen kuliondoa majukumu ya kuzalisha umeme kutoka kwa shirika la Kenya Power ambalo kazi yake kubwa ni ugavi wa umeme. Kenya Power inanunua umeme kutoka KenGen na kuuza kwa watumiaji. Kenya Power nayo iko katika soko la hisa la Nairobi.
Kama hiyo haitoshi, katika jitihada za kuiondolea Kenya Power mzigo wa kujenga, kuendesha na kukarabati miundombinu ya gridi ya taifa, serikali ya Kenya iliunda shirika la Kenya Electric Transmmission Company (Ketraco) mwaka 2008. Kazi yake kubwa ni kupanga, kuchora, kujenga, kuendesha na kukarabati njia kuu zenye msongo mkubwa zinazosafirisha umeme katika gridi ya taifa na kati ya mkoa na mkoa.
Majukumu haya yanagharamiwa na serikali kwa kutumia pesa za kodi ya wananchi na mikopo ya riba nafuu kutoka kwa hisani. Nia ni kuondoa mzigo wa kugharamia ujenzi wa miundombinu mikubwa kutoka kwa Kenya Power na kupunguza bei ya umeme kwa walaji.
Kabla ya hapo ilibidi Kenya Power iwapelekee walaji gharama zote za kujenga na kukarabati miundombinu ya usafirishaji wa umeme kwenye njia kuu za gridi ya taifa. Kwa sasa Kenya Power imebaki na miundombinu inayosambaza umeme majumbani, kwenye ofisi na viwandani.
Muundo huu umefanya mfumo wa usafirishaji umeme nchini Kenya kuwa wa ufanisi mkubwa na umepunguza tatizo la kukatika umeme.
Pia sheria za Kenya zimeruhusu watumiaji wakubwa wa umeme kama vile viwanda kununua umeme moja kwa moja kutoka KenGen. Hii imepunguza tatizo la Kenya Power kuelemewa na mahitaji hasa wakati wa kilele cha matumizi ya umeme. Ripoti mbalimbali zinasema tatizo kubwa la mashirika ya umeme ya umma nchini Kenya kwa miaka ijayo itakuwa ni uhitaji unaopungua, si kuelemewa kwa miundombinu ya usambazaji.
Pamoja na yote hayo Kenya haijamaliza matatizo yake ya umeme. Lakini kuna ufanisi unaoonekana uliofanikishwa na kufanya maamuzi kitaalam na si kisiasa.
Kwa nini Tanzania isijifunze kutoka Kenya?
Isivyo bahati, Tanzania imeshindwa kujifunza kutoka Kenya na nchi nyingine za jirani. Wataalamu wamekuwa wakishauri kuhusu ulazima wa kuligawa shirika la Tanesco vipande vitatu kupunguza mzigo na gharama za uendeshaji na kuleta ufanisi na tija.
Wataalamu wanasema upungufu katika usafirishaji na ugavi wa umeme yataisha au kupungua kwa kiwangokikubwa pale yatakapoundwa mashirika tofauti ya kushughulika na kazi hizo kama ilivyo kwa Ketraco na Power Kenya. Lakini serikali badi haijakubaliana na hoja hiyo ambayo pia imewahi kujitokeza pia katika mijadala ya Bunge.
Wakati akijibu hoja za wabunge Februari 15, 2022 Waziri Makamba aliyataja badhi ya matatizo ya usafirishaji wa umeme.
Alisema njia za umeme zenye msongo mdogo wa 33kV ambazo zinatakiwa zibebe umeme mdogo kupeleka mitaani katika umbali usiozidi kilometa 100 ndizo zinazosafirisha umeme wa msongo mkubwa kwa kilometa zaidi ya 1,000. Kwa mfano njia ya msongo mkubwa ya Dodoma-Kongwa-Mpwapwa-Gairo-Kiteto yenye umbali wa kilometa 1,600 inabebwa na laini ya umeme ya 33kV jambo ambalo ni sababu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara. Njia ya umeme ya 11kV inayopaswa kupeleka umeme majumbani ndani ya kilometa 30 ndiyo inayopeleka umeme Lindi kutoka Dar es Salaam, umbali wa zaidi ya kilometa 100. "Katika hali hii umeme lazima utakuwa unstable [usio wa uhakika]," alisema Makamba. Makamba aliongeza kuwa wizara yake imeshapata Dola za Kimarekani bilioni 1.9 za kukarabati na kujenga miundombinu mipya ya umeme nchini. "Tunaomba muda...tuvumiliane, tupeane muda."
Machi 24 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia Bwana Makamba ameomba Watanzania waipe serikali angalau miaka miwili kuijenga upya miundombinu ya kusafirisha umeme.
Ni hakika kuwa katika suala la umeme nchini Tanzania, muda utaongea. Waziri Makamba anaonekana kuwa ana nia nzuri ya kuboresha upatikanaji wa umeme nchini.
Lakini kama siasa hazitakwisha na kama shirika moja tu la Tanesco litaendelea kubeba mzigo wote wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, waziri mwingine wa Nishati anaweza akarudia maneno ya "tupeane muda" miaka kumi ijayo.
Kukatika kwa umeme nchini Tanzania si tatizo lililoanza jana na ambalo ufumbuzi wake utakuja kwa kuijaza Tanesco 'mapesa'. Tatizo la umeme Tanzania ni la miaka mingi na linatakiwa liangaliwe kwa upana wake na uzito unaostahili.
Uzalishaji wa umeme si tatizo Tanzania
Tanzania ni nchi ambayo imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme, yaani "energy mix." Ina uwezo wa kuzalisha umeme wa maji kwa zaidi ya 4,000MW na umeme wa jotoardhi (geothemal) kwa takribani 5,000MW. Asilimia 10 ya nchi ya Tanzania inafaa kuzalisha umeme wa upepo. Mradi wa kuzalisha umeme kw anguvu ya upepo mkoani Singida haukuwahi kuanza. Nchi nzima inafaa kuzalisha umeme wa jua. Uwepo wa gesi asilia wa zaidi ya futi za ujazo trilioni 60 unamaanisha kuwa uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme kutoka gesi asilia haupimiki. Ifahamike kuwa kwa sasa Tanzania inategemea gesi asilia kuzalisha umeme wake kwa kiasi kikubwa kuliko nishati nyingine yoyote japo bado kuna fursa ya kuongeza uzalishaji huo.
Upatikanaji wa madini ya urani nao pia unaipa Tanzania nafasi ya kuzalisha umeme wa nyuklia kama serikali ikitaka. Tafiti zilizothibitishwa zinaonesha kuwa kuna madini ya urani katika mikoa ya Ruvuma, Dodoma, Singida, Manyara na Arusha japo hayajaanza kuchumbwa.
Kwa kifupi Tanzania haitakiwi kuwa na matatizo ya umeme. Inatakiwa iuze umeme nchi za nje. Lakini rasilimali kama hizi huwa haziwezi kuifaidisha nchi kama siasa zake hazikidhi mahitaji na kuleta tija kwa manufaa ya watu wake.